• UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI


  •   
  • FileName: uhakiki.pdf [read-online]
    • Abstract: sana kama nguzo moja ya kueleza maana ya fasihi. Waitifaki wa nadharia hii hushikilia kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezeka tu ... Kugundua na kutumia kanuni zinazoeleza nguzo za sanaa bora. ...

Download the ebook

Uhakiki wa
Kazi za Fasihi
Mwenda Ntarangwi, Ph.D.
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
Mwenda Ntarangwi, Ph.D.
Augustana College, Rock Island, IL 61201
2004
2
Yaliyomo................................................................ 3
Utangulizi ....................................................... 5
Sura Ya Kwanza
1.0 Fasihi Ni Nini? .............................................. 7
1.1 Fasihi Kama Sanaa Itumiayo Maneno ............. 10
1.2 Fasihi Kama Sanaa: Nadharia Ya Umithilishaji... 12
1.3 Dhana Ya Ubunilizi .......................................... 15
1.4 Dhana Ya Muundo ............................... 16
1.5 Nadharia Ya Uhalisia-Nafsi ................................. 17
1.6 Nadharia Ya Mguso ............................................. 19
1.7 Fasihi Na Jamii ...................................................... 21
1.8 Hitimisho ............................................................. 24
Sura Ya Pili
2.0 Nadharia Za Uhakiki .................................... 27
2.1 Uhakiki Ni Nini? ....................................... 28
2.2 Vigezo Vinavyozingatiwa Katika Uhakiki ........... 30
2.3 Pana Njia Halisi Ya Kuhakiki? ............................... 32
2.4 Nadharia Za Uhakiki ............................................ 35
2.4:1 Nadharia Ya Ki-Marx .......................................... 37
2.4:2 Nadharia Ya Uasilia ............................................ 39
2.4:3 Nadharia Ya Umuundo ...................................... 40
2.4:4 Nadharia Ya Umuundo-Mpya ............................. 43
2.4:5 Nadharia Ya Ufeministi ......................................... 45
2.4:6 Nadharia Ya Uhalisia ............................................ 48
2.4:7 Nadharia Ya Uhalisia-Nafsi (Tathimini-Saikolojia) 49
2.4:8 Hitimisho .............................................................. 52
Sura Ya Tatu
3.0 Maendeleo Ya Fasihi Andishi............................... 54
3.1 Tamthilia ............................................................. 54
3.2 Riwaya .................................................................. 59
3.3 Mashairi................................................................ 65
3
3.4 Hitimisho ......................................................... 69
Sura Ya Nne
4.0 Uhakiki Wa Kazi Za Fasihi.................................... 73
4.1 Utangulizi............................................................ 73
4.2 Jukumu La Mhakiki................................................ 75
4.3 Misingi Ya Kuzingatiwa Katika Uhakiki ......... 78
4.4 Hitimisho................................................................. 108
Sura ya Tano
Tamati .................................................................... 109
Marejeleo............................................................... 112
4
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
UTANGULIZI
Kuhakiki kazi ya fasihi ni jambo ambalo huzingatiwa sana na wanafunzi
na walimu shuleni, vyuoni na katika taasisi nyingine ambapo somo la fasihi
hushughulikiwa. Kitendo cha kuhakiki kazi za fasihi si kipya ulimwenguni hata ingawa
zaidi kimehusishwa na fasihi-andishi. Uhakiki umekuwepo tangu binadamu awe na
uwezo wa kuzungumza na kuadhiri maoni na maisha ya wengine. Hivyo basi uhakiki
umekuwepo hata wakati ambapo fasihi-simulizi ndiyo iliyokuwa fasihi ya kipekee katika
jamii ya wanadamu (yaani kabla ya taaluma ya kuandika na kuchapisha kuzua fasihi-
andishi). Kama ilivyo na mazungumzo au matumizi yoyote ya lugha biaina ya
wanadamu huwa panaulizwa maswali ya kutaka kupata fafanuzi na maelezo zaidi kuhusu
jambo husika. Hadhira huuliza maswali ya ufafanuzi kuhusu kazi wanayoshuhudia au
hata kupinga na kukosoa msimulizi wa kazi ile iwapo wanafahamu muktadha, muundo,
mwelekeo, maudhui, na mengineyo ambayo yanajenga usimulizi huo. Hivyo ndivyo
ilivyo na kazi yoyote ya fasihi.
Kazi ya fasihi inakusudiwa hadhira fulani, na ili iwe ya manufaa kwa hadhira
hiyo, ni lazima iwe yazingatia kaida fulani zinazochukuana na utamaduni wa hadhira
hiyo. Kwa hivyo kazi ya fasihi haina budi kutimiza inachotarajiwa kutimiza. Yaani
kutunga kuna kaida na misingi maalum inayotokana na utamaduni wa jamii husika,
ambayo humwezesha yeyote anayeipokea, isoma, au isikiza kuikadirisha, kuibainisha
kama nzuri, mbaya, au mwafaka. Lakini ni vipi tunafahamu kwamba hilo limetokea?
Kutimiza au kutotimizwa kwa kaida hizo hutokea kwa kuzingatia kazi husika katika
kitendo cha kuihakiki. Uhakiki ndio unaotuwezesha kudhibitisha iwapo kazi ya fasihi
inatimiza kaida inazopaswa kutimiza. Na hivyo basi kudhihirisha kwamba utunzi wa
kazi ya fasihi si jambo la kubahatisha bali huwa limefungwa na kaida maalum. Na kaida
hizo ndizo zinazomwongoza mhakiki. Isitoshe, uhakiki hutuwezesha kuielewa na
kuieleza kazi ile ipasavyo.
Ni wazi kwamba mtu hawezi kuhakiki kitu ambacho yeye hakifahamu au hana
habari kukihusu. Ni nia yetu kabla ya kuingilia swala la uhakiki, tuangazie macho dhana
5
ya fasihi ambacho ndicho kiini cha uhakiki. Mswada huu unatarajia kushughulikia
mambo matatu muhimu; kudondoa mambo muhimu kuhusu fasihi, kubainisha nadharia
mbali mbali za fasihi na kuzingatia maendeleo ya mada mbali mbali za fasihi.
6
SURA YA KWANZA
1.0 FASIHI NI NINI?
Fasihi kama dhana, imeelezwa na wengi kwa kuegemea nadharia na mitizamo
mbali mbali. Hata hivyo ni muhimu tufahamu ya kwamba maana inayopewa dhana au
kitu fulani, huwa inachukuana na matumizi ya dhana yenyewe, watu wanaohusika,
mahali dhana hiyo inamotokea, na hata kipindi au wakati husika. Hii ndiyo sababu
twapata maana mbalimbali zikitolewa kuhusu fasihi. Kwa mfano, waandishi wengi wa
Kimagharibi wamesisitiza kwamba fasihi yahusu tu kazi zilizoandikwa. Ndiposa Okot P'
Bitek (1973:18) anasema:
Katika usomi wa kimagharibi, fasihi humaanisha maandishi ya wakati au nchi
fulani, hasa ile yenye kupewa thamani ya juu katika mtindo na uendelezaji wake.
Ufafanuzi huu unaotilia mkazo uandishi walenga kueleza kwamba fasihi ni amali
ya jamii zilizovumbua sanaa ya uandishi.[tafsiri yetu]
Kwa hivyo, fasihi, kulingana na mtizamo huo wa kimagharibi, imechukuana na uandishi,
na hivyo basi fasihi si fasihi mpaka iandikwe. Bila shaka mtizamo kama huu hupuuza
fasihi-simulizi. Ama kwa hakika hiyo hatua ya kuihusisha fasihi na maandishi ni ya
maksuudi inayodhamiriwa kuonyesha fasihi kama amali ya jamii yenye taluma ya
kusoma na kuandika. Ni kile kitendo cha kibinafsi au cha kubagua ambacho hudhamiria
kuonyesha jamii ambazo hazina taaluma ya uandishi kama jamii duni.
Ukweli ni kwamba pamewahi kuwepo na bado zipo kazi za fasihi za hali ya juu
kutoka kwa jamii ambazo hazikuwa na taaluma ya kusoma na kuandika. Isitoshe, pana
mifano kemkem ya kazi zilizokuwa katika masimulizi hapo awali, lakini sasa
zimehifadhika katika maandishi na huratibiwa kama kazi za fasihi. Kazi nyingi za ushairi
7
wa Kiswahili ni mifano ya kazi kama hizo. P'Bitek (1973:20) kwa kuipinga kauli ya
kutengea fasihi jamii fulani anasema;
Tunashurutika kukataa ufafanuzi huu unaotenga na kubagua; na badala
yake kuunda ufafanuzi wa kimapinduzi utakaoionyesha fasihi kama
inayochukua kazi zote za kubuniwa za wanadamu zinazoelezwa kwa
maneno. [tafsiri yetu]
Maneno haya ya P’Bitek ni maneno ya kuvutia lakini huenda yasiwe na dharura yoyote
katika wakati huu maana pana kazi kemkem za fasihi katika tamaduni zetu ambazo
wakati wa awali hazingeorodheshwa kama kazi za fasihi. Lakini bado hatujatoa
mwongozo thabiti wa kuonyesha ni kazi zipi zinaratibiwa kama za fasihi na ni zipi
zinazoingia katika kikundi chengine. Ni dhamira ya mswada huu kuangazia jambo hili
macho ili kuchanganua ni kazi za aina gani zapaswa kuchukuliwa kama kazi za fasihi iwe
andishi au simulizi.
Waandishi wengi wameandika kuhusu swala hili la fasihi, na maoni yao huwa
kwa njia moja au nyengine yanadhihirisha kutotosheka kwao na yaliyosemwa na wengine
kuhusu swala hilo, wengine wakijaribu kubainisha utunzi uliopo, na wengine
wakifafanua zaidi maelezo yaliyopo. Ameir Issa Haji (1983:30) anasema kuwa fasihi ni:
Sanaa itumiayo maneno ili kutoa picha halisi ya mwanadamu akiwa
maishani mwake; mahusiano yake na viumbe wengine, migogoro yake na
mazingira, shida zake, raha zake, matumaini yake na jinsi anavyopiga
hatua katika maendeleo yake.
Mtizamo kama huu waitizama fasihi kama kazi inayoendelezwa kwa maneno, iwe
andishi au simulizi [kuandika na kusimulia ni mtambo tu wa kuiwasilisha kazi hiyo].
Kuandika sawa na kuchonga au kuchora ni njia ya kueleza dhana tu, na jinsi ambavyo
mchoraji hutumia rangi katika kazi yake, mtunzi wa kazi ya fasihi hutumia maneno
kueleza dhana na hisia zake. Maneno hayo huenda akayaandika, akayaimba au
akayazungumza. Kwa hivyo, fasihi iwe imeandikwa au imesimuliwa bado ni fasihi.
8
Naye Odaga (1985:xxi) anasema kwamba;
Fasihi ni sanaa ambayo mtambo wake ni neno na
kiini chake ni binadamu. (Tafsiri yetu)
P’Bitek (kama hapo juu) anasema;
Fasihi husimamia kazi zote bunifu anazozitumia
mwanadamu kujieleza kwa maneno ambayo yaweza kuimbwa,
kusemwa, au kuandikwa. (Tafsiri yetu)
Toleo la kumi na nne la Compton’s Encyclopedia (1974:305) yaeleza fasihi kwa njia
pana huku fasihi ikichuliwa kama;
iliyo zaidi ya lugha. Ni dhana na hisia
zilizovingikwa katika muziki wa lugha.
Na huchukua umbo la maneno na picha
zilizowekwa pamoja na ubunifu. Fasihi
ni jinsi ya kuona, kuhisi, kufahamu.
(Tafsiri yetu)
Kwa muhtasari twaweza kusema kwamba pana kauli hizi za kimsingi ambazo hujitokeza
katika fafanuzi za wataalam hawa na wengine wengi kuhusu dhana ya fasihi:
- Fasihi ni sanaa inayodhihiri ubunifu
- inayotumia maneno kuwasilisha mambo yake
- na ambayo hulenga binadamu kama kiini chake n.k.
Kama tulivyotaja hapo awali maana ya neno au dhana yoyote hutegemea mambo
mengi na hivyo basi fasili hii yetu ya fasihi huenda isichukuane na maoni ya mwingine
anayechagua kuitazama fasihi kwa njia tofauti. Lakini hata mhakiki atumie mtizamo
gani, fasili yake pamoja na hitimisho lake litategemea anachukua fasihi kumaanisha nini
9
pamoja na jukumu la mtunzi wa fasihi hiyo. Katika misingi hii, huenda likawa jambo
mwafaka kuzingatia baadhi ya vigezo vilivyowahi kutumiwa katika kufafanua fasihi ili
tupate msingi wa kufanya uhakiki.
Pametokea vigezo tofauti vya kuifafanua fasihi kutegemea msisitizo anaotaka
kuweka mfasili pamoja na maendeleo na mabadiliko ya maisha kihistoria. Kuna wale
wanaosisitiza umbo la nje la fasihi ambao wamekita nadharia zao katika muundo huo
ilhali wengine wanasisitiza umbo lake la ndani. Pana wale wanaochagua kuzingatia
wahusika katika kutungwa kwa kazi hiyo, yaani mtunzi, hadhira yake na hata athari za
jamii. Ndiposa twapata vigezo vilivyotumiwa ama vyalenga maumbo ya fasihi, maudhui
yake au yote mawili.
Ni muhimu kueleza kwamba hivi vigezo tutakavyovitaja hapa, mara nyingi
vimejitokeza katika utanzu wa uhakiki, hivi kwamba maelezo ya 'fasihi ni nini'
yanatumiwa kutathimini kutimizika kwa masharti yanayozingatiwa na mtunzi anapotunga
kazi yake. Kwa hivyo kama utunzi wa fasihi husisitiza maudhui mbali mbali basi huenda
mhakiki akatumia kigezo hicho hicho katika kazi yake ya uhakiki kubainisha kufaulu
kwa kazi hiyo katika lengo hilo.
Sasa tuangalie baadhi ya vigezo vinayotumiwa katika kuifafanua fasihi.
1.1 FASIHI KAMA SANAA ITUMIAYO MANENO
Aghalabu, wataalamu wametumia kigezo cha `neno' kama njia ya kutofautisha
fasihi na sanaa nyingine kama vile uchoraji na uchongaji. Wanasema kwamba fasihi ni
sanaa inayotumia maneno ili kuwasilisha maudhui na hoja zake. Wataalamu
wanaoshikilia kigezo hiki ni wale wanaopinga kauli ya kimagharibi ya kuhusisha fasihi
na taaluma ya maandishi.
Kwa hivyo, tunaposema kwamba fasihi ni sanaa inayotumia maneno huwa tayari
tumeliacha wazi swala kuhusu maneno yaliyoandikwa au yaliyosimuliwa. Neno, liwe
limeandikwa au limetamkwa, ni neno. Lakini sio kila neno huenda likaorodheshwa kama
fasihi. Fasihi huwasilishwa kwa maneno lakini maneno hayo hutumiwa kwa njia maalum
ili kuyatenganisha/kuyabainisha na maneno ya kawaida. Kwa hivyo lazima pawe na sura
maalum zinazounda maneno ya fasihi ili kuyatofautisha na maneno ya kawaida. Ili
kujitandua kutoka katika utata huu, ni muhimu kuichukulia fasihi sio kama maneno bali
10
kama sanaa itumiayo maneno. Na matumizi ya maneno hayo katika fasihi huashiria
usanii wa namna fulani. Usanii huo ndio unaofanya maneno ya fasihi yawe tofauti na
maneno ya kawaida japo mofolojia na fonolojia yake ni sawa. Maneno yanayotumiwa
katika fasihi ni maneno zaidi ya maneno mengine kwani yanatumiwa kisanaa. Lakini
hamna maneno maalum yaliyotengewa fasihi na ambayo hayapatikani katika utanzu
mwingine wowote wa maisha ya jamii. Ukweli ni kwamba katika fasihi, maneno ya
kawaida hutumiwa kisanaa.
Kirumbi P.S (1975:10) anatutolea mfano wa jinsi maneno yanaweza kutumiwa
kisanaa. Ametutolea mifano miwili ya shukrani zilizotolewa na watu wawili tofauti;
wa kwanza anasema:
Ndungu mpenzi,
Nimepokea msaada wako nami umenisaidia sana sikutazamia kupata
msaada katika shida hii iliyonikuta. Ama Mungu mkubwa. Ndugu, asante
sana kwa msaada wako. Kwa kweli nakushuru sana tena sana.
Mungu akubariki.
wa pili naye anasema:
Ndugu,
Sijasikia mkono ukipewa shukrani na mguu kwa kuutoa mwiba - lakini ni
ujinga wa mguu kufikiria unastahili kutolewa mwiba, maana kuna miili
isiyo na mikono, na miguu hiyo ichomwapo na miiba hutaabika sana.
Hivyo sioni kustahili kwangu bali ni rehema na neema kuwa na ndugu,
nami nimepata na kujifunza zaidi upendo wako.
Watu hawa wawili wametendewa jambo la kuwafaa na wote wametumia maneno kutoa
shukrani zao. Hata ingawa ujumbe wa maneno yao ni mmoja, twaona kuwa maneno ya
mmoja ni ya kisanaa ilhali ya mwingine ni ya kawaida. Maneno hayo yanapatikana
katika msamiati wa jamii husika lakini jinsi yalivyoteuliwa na kutumiwa ndipo tofauti
inatokea. katika mfano wa pili kwa mfano, mtunzi anachagua kufananisha kitendo
11
alichotendewa na ndugu yake na kitendo cha mkono kuondoa mwiba mguuni. Mguu
unapochomwa ni mwiba huumia na huhitaji kuondelewa (kusaidiwa), kwani hauwezi
kujitoa mwiba ule wenyewe. Hivyo ndivyo ilivyo katika fasihi; kwamba maneno
hutumiwa kwa njia maalum (ya kisanaa) inayotoa mguso fulani kwa hadhira.
Wakati mwingine kazi ya fasihi huweza kuendelezwa kwa matendo badala ya
maneno. Kwa mfano tamthilia huhusisha maneno na matendo pamoja ili kuwa kamili.
Bila matendo, tamthilia haijakamilika. Kwa hivyo huenda maneno yakawa nguzo moja
tu ya fasihi na kama sivyo, tamthilia itaachwa nje ya fasili ya fasihi. Lakini ni muhimu
kukumbuka kwamba hata hayo matendo katika tamthilia huweza kueleweka katika
misingi ya maneno. Kwa hivyo kiini cha fasihi ni maneno. Na maneno hayo
yanatumiwa kisanaa.
1.2 FASIHI KAMA SANAA: NADHARIA YA UMITHILISHAJI
Njia moja ambayo pengine ni kongwe sana na iliyopata kutumiwa kufafanua
fasihi kama sanaa ni ile ya kuiona fasihi kama aina ya umithilishaji. Kwa mtizamo huu,
fasihi hufafanuliwa katika uhusiano wake na maisha; kwa kuiona kama njia ya kujenga
tena au kuhuisha tukio au hali fulani ya maisha kwa kutumia mchoro na rangi. Huu ni
mtizamo ulioendelezwa na Aristotle na kufuatiliwa na wafuasi wake. Abrams M.H
(1981) anasema hivi kuhusu umthilishaji;
Katika kazi yake ya `Poetics', Aristotle anaeleza ushairi kama umithilishaji
wa vitendo vya mwanadamu. Kwa `umithilishi' anamaanisha `uwakilishi',
kwa msingi yake. [tafsiri yetu]
Kwa hivyo kwa maoni ya Aristotle, shairi humithilisha kwa kuchukua kitendo fulani cha
mwanadamu na kukionyesha upya katika `mtambo' mpya - ule wa maneno.
Mtizamo huu wa kuiona fasihi kama sanaa ya umithilishaji waweza kufasiriwa
kwa njia mbili kuu; kwanza, twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba
fasihi hujaribu kuiga na kumithilisha maisha; yaani maudhui ya fasihi ni tajiriba za watu
12
waishio. Lakini pendekezo kama hili lazua matatizo kwani hatusemi mengi kuhusu fasihi
kwa vile hatutilii maanani kile kinachofanyiwa hayo maudhui. Pia kwa kutumia neno
`maisha' twaweza kuuchukulia kijuujuu na kupendekeza kwamba fasihi ni tajiriba za
watu waishio. Pia kwa kutumia neno `maisha' twazua utata mkubwa kwani maisha ni
kitu tofauti kwa watu tofauti kwani kila mmoja japo wanishi katika mazingira sawa,
aghalabu huguswa na mambo kwa njia tofauti. Pili, twaweza kusema kwamba maisha
yanaigwa kwa njia ambayo yanaumbwa upya na kutafsiriwa upya kwani hapawezekani
kuondoa kitu kutoka mtambo mmoja na kukiingiza katika mtambo mwingine bila
kukiadhiri au kukibadilisha. Dhana hii ya pili inakaribiana na mojawapo ya sura muhimu
katika fasihi; ile ya kwamba malighafi ya fasihi huundwa upya na hata kubadilishwa.
Lakini bado hatuonyeshi ni mambo gani ya maisha humithilishwa. Kuhusiana na hali hii
welleK na Warren (1949:95) wanasema;
Iwapo inachukuliwa kwamba fasihi, kwa wakati wowote ule, humulika
hali ya kijamii iliyopo kwa uhalisi wake, basi hiyo si kweli; ni wazi, vile
vile, kwamba si kweli kusema fasihi hudhihirisha baadhi ya uhalisi uliopo
katika jamii. [tafsiri yetu]
Kwa hiyo, kwa maoni ya wataalamu hawa wawili kauli ya kuiona fasihi kama
umithilishaji wa maisha ni ya kupotosha. Wanaendelea kutaja kwamba;
Fasihi kwa hakika si picha ya mkondo wa maisha, bali ni ufupisho na
muhtasari wa historia nzima. [tafsiri yetu]
Wanalosisitiza hapa ni kwamba fasihi si picha ya moja kwa moja ya maisha bali ni
muhtasari wa maisha na matukio yake. Lakini na wao hawatuelezi ni vipi fasihi
yatofautiana na kumbukumbu iliyoandikwa kuhusu maisha na mwanahistoria. Ni
kwamba kazi ya fasihi huzingatia kaida maalum zinazotawala kila utanzu wa fasihi na
kuibainisha na kazi ya mwandishi wa historia kwa mfano.
Hata hiyo Wellek na Warren (1949:102) wanakiri kwamba, “hatuwezi kupuuza
wazo kwamba picha fulani ya maisha huweza kupatikana katika fasihi [tafsiri yetu].”
13
Pana kauli moja ambayo yajitokeza katika kigezo hiki cha kuiona fasihi kama sanaa
inayomithilisha maisha. Katika umithilishi huu mtunzi anatumia maneno. Lakini katika
dhana hii ingawa yasemekana kwamba fasihi huhusu maisha, hatuambiwi ni kwa
kiwango gani. Hata hivyo mfumo huu unaotokana na nadharia ya umithilishaji umekuwa
nguzo kwa kazi nyingi za fasihi na zisizo za fasihi. Abrams, M.H (1981) anasema;
Hata ingawa nadharia ya umithilishaji ilififia, ilichukuliwa tena ni R.S
Crane na wahakiki wengine wa Chicago waliotumia misingi ya kiaristotle
katika tathimini zao. Wahakiki wengi wa ki-marx huiona fasihi kama
umithilishaji. (Tafsiri yetu)
Kwa hivyo hata ingawa pana wale wanaopinga kuwa fasihi ni umithilishaji, kauli hii
inatoa nguzo kwa mitizamo mingine kuhusu fasihi. Twaweza kusema kwamba pana
uhusiano mkubwa kati ya umithilishaji na uhalisia (jambo ambalo huhimizwa sana katika
baadhi ya kazi muhimu za fasihi).
Kazi nyingi za fasihi huweza kuhusishwa na umithilishaji. Methali na vitendawili
ni tanzu za fasihi simulizi ambazo zinatumiwa sana na jamii kwa shughuli mbali mbali.
Twapata kwa hakika kwamba jinsi methali zilivyo ni mfano halisi wa umithilishaji kwani
dhana inayosimamiwa na methali huwakilisha hali halisi ya maisha. Maneno
yanayojenga methali, vitendawili na hata misemo ni mfano wa aina fulani ya
umithilishaji. Methali kama vile `mwamba ngoma ngozi huivutia kwake' imeundwa
kama mithili ya moja kwa moja ya maisha ya mwanadamu. Kwamba mtu anapovuta
ngozi wakati anapounda ngoma huwa anaivutia upande wake, (huo ni ukweli wa mambo)
na hawezi kuivuta ikaendea mwenzake kwani itapuuza dhana ya kuvuta. Kwa hivyo kiini
cha methali hii ni ukweli halisi wa mambo. Hivyo basi pana hali ya umithilishaji katika
utanzu huo wa fasihi.
Kwa jumla twaona kwamba fasihi ni sanaa ambayo yaweza kuelezwa kama
inayomithilisha. Umithilishaji huu hata hivyo si wa moja kwa moja kwani kama
ingekuwa hivyo, basi hapangekuwa na tofauti kati ya fasihi na historia. Hapo ndipo
twaingilia kigezo cha tatu cha kuieleza fasihi.
14
1.3 DHANA YA UBUNILIZI
Hata ingawa kazi ya fasihi kwa kawaida huwa yamithilisha au kujaribu kuumba
upya maisha kwa njia moja au nyengine, twatambua ukweli kwamba yaliyotungwa si
maisha halisi moja kwa moja. Kwa mtizamo huu yaelekea kwamba fasihi si maisha
halisi bali ni tokeo la ubunifu wa mtunzi, yaani mtunzi ana uwezo wa kubuni visa na
wahusika wake kwa njia ambayo haikanganyi hali halisi ya maisha.
Hata hivyo, ubunifu huu lazima uongozwe na kaida za hali halisi ya maisha yaani
kama asemavyo Horace (1975:103):
Chochote utakachochagua kwa minajili ya kupendeza, hakikisha kwamba
kipo karibu na ukweli. [tafsiri yetu]
Yaani mtunzi anapaswa kuufanya ulimwengu wake wa kubuni kuwa picha halisi ya
maisha katika ukamilifu na ukweli wake, hata ingawa alivyoyashughulikia ni ya kubuni
tu. Horace (1975:95) anafafanua zaidi kauli hii asemapo kwamba;
Washairi na wachoraji wamekuwa wakifurahia uhuru wa utunzi na
kufanya majaribio jinsi watakavyo. Hili nalifahamu, na mimi kama
mshairi hufurahia uhuru huo; lakini si kwa kiwango ambacho kwacho
viumbe visivyotangamana vinawekwa pamoja, hivi kwamba ndege na
nyoka wanawekwa pamoja, wanakondoo pamoja na simba marara. [tafsiri
yetu]
Anachosisitiza Horace ni kuwa, hatuwezi kumnyima mtunzi uhuru wa kubuni, lakini
mtunzi akumbuke kwamba ubunifu wake usikiuke kaida zinazotawala maisha halisi ya
jamii. Kumpa mtunzi uhuru wa ubunifu na kisha umtarajie afuate kaida fulani ni
kumnyima uhuru kamili. Kama mtunzi atakanganya hali halisi ya maisha kama mbinu
yake ya kutunga, basi na tumpe uhuru huo alimradi kazi yake twaielewa kwa mtizamo
huo. Kwa hivyo, fasihi si kazi inayohusu mambo ya kipekee bali ni uwasilishaji wa
15
maisha ya jamii kwa njia bunifu isiyo ya moja kwa moja. Ndiposa Aristotle (1975:103)
anasema:
Ni wazi kwamba, si jukumu la mshairi kuendeleza yaliyotokea bali
huendeleza yanayoweza kutokea-yaani kinachoweza kutokea katika
msingi ya haja au uwezekano. [tafsiri yetu]
Hapo ndipo fasihi hutofautiana na historia kwani wakati fasihi huendeleza linaloweza
kutokea, historia huendeleza kilichotokea; na fasihi ikieleza lililotokea hulieleza kisanaa,
sio moja kwa moja. Hivyo basi, fasihi ni utanzu unaoendeleza maisha kwa njia bunifu
iliyojikita katika msingi na kaida zinazotawala maisha halisi.
1.4 DHANA YA MUUNDO
Ili kueleza maana ya fasihi, wataalamu wengi wamejaribu kuzingatia baadhi ya
vigezo vinavyoitambulisha, hasa ikiwekwa katika mkabala mmoja na tanzu nyengine za
maisha ya jamii. Twaweza kusema kwamba dhana ya ubunilizi ni njia nzuri ya
kutofautisha fasihi na uhalisia pamoja na ulimwengu halisi. Lakini kupitia kwa dhana hii
hatujaelezwa hasa kinachofanyiwa malighafi ya kazi ya fasihi. Ili kutimiza hilo, dhana
nyengine imependekezwa; kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuchukuliwa kama muundo,
kama mpangilio maalum. Kila kazi imepangwa kwa hali ya juu sana na viungo vyake
vinategemeana hivi kwamba kazi kamilifu huwa ni mwafaka zaidi kuliko kiungo chake
kimoja. Aristotle amelizungumzia swala hili hata ingawa anazingatia zaidi ploti.
Aristotle (1975:29) anasema:
Chombo kizuri, kiwe kiumbe au kitu kizima kilichojengwa kwa vipande.
kazi ya fasihii yapaswa kutolewa kama kitu kimoja. Ploti, kama mithili ya
kitendo, lazima imithilishe kitendo kimoja; na muungano wa vipande vya
kitu kizima uwe hivi kwamba kipande kimoja kikiondolewa pale, kile kitu
kizima hutengana. Kwani kipande ambacho hakitoi athari kiondolewapo,
bila shaka si kipande halisi cha kizima. [tafsiri yetu]
16
Tukitizama fasihi kwa njia hii, tunatambua umoja na uwiano wa kila kazi unaoifanya
ieleweke na iwe na muundo maalum. Hivyo basi kazi ya fasihi ni muundo wa vipande
vinayopatana na kuhusiana ili kujenga kitu kimoja. Hivyo basi kipande kimoja cha kazi
hiyo huwa hakina maana yoyote kivyake mpaka kihusishwe na vingine.
Kama ambavyo dhana ya ubunilizi hutusaidia kutofautisha fasihi na matukio
halisi maishani, dhana ya muundo hutuwezesha kutofautisha fasihi na matumizi mengine
ya lugha. Inatutolea ile hali ya usababishano, kwamba kazi ya fasihi ni utungo ulioundwa
kwa visa vinavyowiana hivi kwamba kimoja hutangulia chengine. Pia, kisa kimoja
hutokea ili kusababisha chengine na vyote vinahusiana kwa njia ambayo kimoja hakiwezi
kueleweka bila chengine. Haya yote yanawezekana kupitia lugha inayotumiwa. Kwa
hivyo katika muundo, tunazingatia jinsi lugha inavyotumiwa. Kwa ufafanuzi zaidi
kuhusu lugha katika fasihi rejelea sehemu ya `fasihi kama sanaa itumiayo maneno'.
Mpaka sasa tumekuwa tukizingatia vigezo vya kuainisha fasihi ambavyo twaweza
kuviita vya umbo la ndani. Sasa tutaingilia umbo la nje la fasihi hasa kwa kuzingatia
mtunzi wake pamoja na hadhira yake.
1.5 NADHARIA YA UHALISIA-NAFSI
Kigezo kingine kinachotumiwa katika kuianisha fasihi ni kuiona fasihi ile kama
zao la mtunzi binafsi. Fasihi kwa mtizamo huu huzingatia saikolojia na sifa za mtunzi
huyo. Kigezo hiki kimezingatiwa hasa katika nadharia ya tathimini saikolojia . Ni wazi
kwamba chanzo cha kazi ya sanaa ni yule anayeiumba, yaani mtunzi wake, na hivyo basi
maelezo yanayopatana na hulka na maisha ya mtunzi yamezingatiwa kwa muda mrefu
sana kama nguzo moja ya kueleza maana ya fasihi.
Waitifaki wa nadharia hii hushikilia kwamba kazi ya fasihi yaweza kuelezeka tu
iwapo itazingatiwa kwa mkabala mmoja na maisha ya mtunzi wake. Hivyo basi fasihi
huonekana kama kielelezo cha uhalisia wa maisha, jinsi yanvyotafsiriwa na nafsi ya mtu
bila kujali ukweli kama unavyodhihiri kwa nje. Jinsi mtunzi anavyojieleza kupita kazi ya
fasihi linakuwa jambo muhimu katika nadharia hii.
Katika mtizamo huu huu, fasihi imezingatiwa kama hisi; yaani ni kielelezo cha
hisi za mtu binafsi (mtunzi). Jinsi mtu anavyoona na kuyahisi maisha linakuwa jambo la
kuzingatiwa kama fasihi. Wataalam wa jadi wa fasihi kama vile Aristotle wanashikilia
17
wazo hili hili kuhusu fasihi. Aristotle aliamini kwamba fasihi au ushairi hasa ni utanzu
ambao kwao binadamu hutoa hisia zake za ndani kuhusu maisha. Hivyo basi ushairi
ukawa ni kielezo cha uhalisia wa nafsi ya mtunzi, jambo ambalo limezingatiwa katika
kueleza fasihi ni nini.
Hata wahakiki wanaozingatia nadharia ya tahakiki-saikolojia kama vile Sigmud
Freud wanashikilia kwamba kazi ya fasihi ni kielezo cha ndoto na matamanio
yasiotimizwa ya mtunzi. Yaani kazi ya fasihi si chengine bali imejaa ndoto za mtunzi
pamoja na majaribio ya kutimiza matamanio yake. Kwa mtizamo huu, fasihi ni hisi, hisia
na mataminio ya mtunzi; yaani maisha yake. Hapa ndipo twapata hata biografia
zikichukuliwa kama kazi za fasihi.
Mtizamo kuu kuhusu fasihi haujapokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya
wataalam. Jefferson (1982:99) anasema:
Utunzi na usomaji wa fasihi hauna uhusiano wowote na nafsi halisi ya
mtunzi na fasihi huwepo bila kutegemea mazingara halisi pamoja na hulka
ya mtunzi. [tafsiri yetu]
Kwa hivyo, kazi ya fasihi haina uhusiano wowote na nafsi ya mtunzi wake. Anasema
kuwa kazi ya fasihi hujisimamia yenyewe kama kazi ya fasihi na haihitaji kuhusishwa na
mtunzi wake ili kueleweka ama kutungwa. Lakini hatuwezi kulitupilia mbali wazo hilo
kwani kila kitendo cha kutunga hutokana na fikira, maoni, tajiriba, na hisia za mtunzi,
jambo ambalo lina ubinafsi maalum unaodhihiri, japo kwa kiwango duni, hulka ya
mtunzi huyo.
Nao Wellek na Warren (1949:78) wana maoni haya kuhusu mtizamo huo wa
fasihi:
Wazo kwamba sanaa kwa ujumla ni uhalisia-nafsi unaotoa hisi
na tajiriba za mtu, ni la kupotosha. Hata panapotekea
uhusiano wa karibu sana kati ya sanaa na maisha ya mtunzi,
hili lisichukuliwe kumaanisha kwamba sanaa ni mwigo wa
18
maisha. Mtizamo huu husahau kwamba kazi ya sanaa ni kazi
kivyake wala si kusanyiko la tajiriba za mtunzi. [tafsiri yetu]
Maoni ya wataalum hawa yanadhihirisha wazo la awali kwamba fasihi ni kazi
inayojisimamia na iliyo na kaida zinazoitawala. Hivyo basi, tamthilia, riwaya au shairi
huwa zinaongozwa na kutawaliwa na kaida za kifasihi zinazohusu kila utanzu.
Tukichunguza mtizamo huu kuhusu fasihi twaona kwamba unapuuza baadhi ya hoja
halisi za kimantiki. Kazi ya sanaa huenda ikawa si maisha halisi ya mtunzi bali ni maoni
au mtizamo wake kuhusu maisha. Huenda ikawa pia ni kinyago cha kuficha nafsi yake
halisi au huenda ikawa picha ya maisha anayotaka kuyakimbia. Isitoshe, tusisahau
kwamba huenda tajiriba ya maisha halisi ya mtunzi ikawa tofauti na ile ya sanaa; yaani
tajiriba halisi maishani hutizamwa kwa jinsi ambavyo zitafaa fasihi na huwa kwa kiasi
fulani zimeongozwa na kuathiriwa na kaida za kisanaa zinazotawala kazi yake. Ama
kweli kazi ya fasihi inayoorodhesha matukio kama yalivyo bila usanii si sanaa bali ni
kumbukumbu au historia.
Hata hivyo hatuwezi kupuuza kabisa kigezo hiki kwani kinachangia katika
kueleza fasihi ni nini. Lililo muhimu kutambua ni kwamba kigezo hicho hakiwezi
kutumiwa peke yake kueleza fasihi ni nini. Ni lazima kihusishwe na vigezo vingine
mbali mbali ili kutoa picha kamili na pana ya fasihi.
1.6 NADHARIA YA MGUSO
Mtizamo mwingine kuhusu fasihi ambao twaweza kuuita wa umbo la nje ni
kuitizama fasihi katika uhusiano wake na umma wake ambapo msisitizo unatiliwa mguso
unaotolewa na kazi ya fasihi kwa hadhira yake. Kila kazi ya fasihi hulenga kwa njia
moja au nyengine mtu au watu fulani (hadhira) hata kama hadhira hiyo ni nafsi ya mtunzi
husika. Kazi ya fasihi hutoa mguzo wa aina fulani kwa hadhira ili ifikirie na kujiuliza
maswali au hata kutoa funzo fulani.
Kwa kuunga mkono maoni haya, Vasquez, A.S (1973:113) anasema:
.... kazi ya sanaa huathiri watu na inachangia katika kuhimiza au
kupuuza dhana zao, maazimio yao, hata maadili
yao - ina msukumo wa kijamii ambao huathiri watu kwa nguvu
19
zake za kihisia na kiitikadi. Ama kwa hakika, hakuna
anayebaki vile vile baada ya `kuguswa' na kazi ya halisi ya sanaa.
[tafsiri yetu]
Kuna nyakati ambapo imependekezwa kwamba hadhira hutekwa kabisa na wahusika
katika kazi ya fasihi mpaka hadhira hiyo ikajitambulisha na wahusika hao kiasi cha
kupoteza utambulishi wake asilia, hata kama ni kwa muda tu. Hata Wellek na Warren
(1949:102) wana maoni yayo hayo wasemapo:
Watu wamewahi kubadilisha mienendo yao katika maisha kwa kuathiriwa
na wahusika wa kubuni katika fasihi. [tafsiri yetu]
Tunachokisisitiza hapa ni wazo lile lile kwamba kazi ya fasihi hutoa mguso kwa hadhira
yake, na huu mguso ndio unaotumiwa kama kigezo cha kueleza maana ya fasihi.
Ndiposa twapata wataalamu wengine wakisema kuwa fasihi ni kazi ya kufurahisha.
Horace (1975:103) anasema “washairi hulenga kusaidia au kufurahisha msomaji, au
kusema kile kinachopendeza na wakati huo huo kusema kinachofaa [tafsiri yetu].”
Tatizo linalozuka katika mtizamo huu ni kwamba ni vigumu kusema kama kweli
pamesababika au kutokea mguso wowote kwa hadhira baada ya kusikiza, kuona au
kusoma kazi ya fasihi. Mguso aghalabu ni jambo la kihisia na kibinafsi na huwa vigumu
sana kutathiminiwa. Isitoshe, yahitajika kupima na kutathimini kiwango cha mguso huo,
kama upo, ili kupata hitimisho lenye mashiko. Jambo hili huenda likawa gumu sana
kutimizwa. Lakini iwapo ni watu ambao tunawafahamu ni rahisi kuthibitisha kama
wamebadili maoni au mienendo yao kuhusu jambo fulani ambalo limegusiwa katika kazi
ya fasihi.
Baada ya kuorodhesha vigezo hivi mbali mbali vinavyotumiwa kueleza fasihi,
pana jambo ambalo linadhihirika kila mara na katika kila kigezo -- kwamba fasihi ina
uhusiano mkubwa na jamii, na hakuna fafanuzi moja inayoweza kusimamia kazi zote za
fasihi, kila moja yategemea muktadha na dhamira ya mfafanuzi. Haya tuliyoyatoa hapa
ni maongozi ambayo yanaweza kusaidia katika kuielewa fasihi kama dhana pana lakini
iliyo na sura maalum zinazotambulika. Tungependa kupitia dhana hii ya fasihi na jamii
20
kwa sababu mbali na kuwa muhimu katika kazi yetu, dhana hii imetumiwa pia katika
kueleza maana ya fasihi.
1.7 FASIHI NA JAMII
Fasili nyingi za fasihi zimeegemea kuileza katika uhusiano wake na jamii. Fasili
hizi zimeonyesha kwamba fasihi ni taasisi ya jamii na uhusiano wake na jamii hauwezi
kupuuzwa. Mmoja wa wanaounga mkono dhana hii ni Escarpit, R (1974:4) anayesema
kwamba:
Fasihi lazima ichukuliwe kama iliyo na uhusiano
usiotatanika na maisha ya kijamii.[tafsiri yetu]
Fasihi ni taasisi ya kijamii, inayotumia lugha (ambalo ni zao la kijamii) kama mtambo
wake. Isitoshe, imesemekana (na ni kweli) kwamba fasihi huwakilisha maisha. Maisha
kwa upana wake huhusu uhalisi wa kijamii, hata ingawa ulimwengu halisi na hata
ulimwengu wa ndani wa mtu binafsi ni mambo yanayoweza kuzingatiwa katika fasihi.
Mbali na hayo twafahamu kwamba iwapo fasihi hulenga watu fulani, basi bila shaka hiyo
fasihi yahusu jamii fulani lau sivyo hapana haja kutungia watu kazi isiyowahusu ndewe
wala shikio.
Jambo lingine la kutaja hapa ni kwamba mtunzi mwenyewe ni mwanajamii kwa
ambavyo ana nafasi na tabaka fulani katika jamii yake; yeye hutambuliwa na jamii kama
mmoja wao. Hawezi kuepuka nafasi hiyo yake katika jamii wala hawezi kukwepa athari
ya jumuiya katika utunzi wake kwani kama mtoto mchanga yeye anafundishwa maadili
na itikadi za jamii yake ili kuweza kuenea katika jamii hiyo. Na kama ambavyo tumetaja
tayari, mtunzi hulenga hadhira fulani hata iwe ndogo vipi.
Mara nyingi fasihi hutokana na uhusiano wa karibu sana na taasisi maalum za
kijamii. Taasisi za kiuchumi, kisiasa, na kijamii zimekuwa na uhusiano mkubwa sana na
utoaji wa fasihi na kila kazi ya fasihi kwa njia moja au nyengine, hudhihiri ukweli huu.
Maendeleo na mabadiliko ya jamii yametokea kuwa maendeleo na mabadiliko ya fasihi
hivi kwamba hatuwezi kutenganisha fasihi na jamii inamoibukia. Uhusiano huu unatokea
kwa sababu pindi maisha ya jamii yabadilikapo, mielekeo, tamaduni na hata maadhili ya
21
jamii hubadilika pia. Aidha, mabadiliko ya fasihi toka simulizi hadi andishi ni zao la
mabadiliko katika maisha ya jamii ambapo taaluma ya kusoma na kuandika ilitokea.
Kwa hivyo fasihi inalo jukumu kuu katika jamii ambalo sio la kibinafsi, bali ni la kijamii.
Katika kuiunga mkono kauli hii, Wellek na Werren (1949:95) wanasema kwamba:
Uhusiano kati ya fasihi na jamii hujadiliwa kwa kuanza na
kaulo aliyoitoa De Bonald kwamba `fasihi ni kielelezo cha
jamii'.[tafisiri yetu]
Kwa hivyo ni muhimu kuichukulia fasihi kama zao la jamii ambalo pia huathiri na
kuathiriwa na jamii.
Hata katika nyingi za tahakiki za fasihi ambazo twaweza kuziita za kijamii (kama
za Ki-marx) pamesisitizwa kauli kwamba mtunzi anapaswa kuendeleza maisha ya wakati
wake kwa ujumla wake; kwamba anapaswa kuwa kiwakilishi cha wakati wake na jamii
yake. Kwa maoni ya waitifaki wa tahakiki hizi, `uwakilishi' huelekea kumaanisha kuwa
mtunzi anapaswa kutambua na kuona hali halisi za maisha katika jamii yake na
kuzizingatia katika utunzi wake. Maoni ya Hegel na Taine katika Wellek na Warren
(1949:95) ni mfano unaochangia zaidi kauli hii wanaposema:
Katika uhakiki wa Kihegel na hata ule wa Taine, utukufu wa kijamii na wa
kihistoria huenda sambamba na utukufu wa kisanaa. Msanii huendeleza
ukweli, na huo ukweli ni wa kijamii na kihistoria. [tafsiri yetu]
Tunaloweza kuongeza ni kwamba pana tatizo linalokumba juhudi yoyote ya
kujaribu kutenganisha fasihi na jamii kwani fasihi huathiriwa na mandhari ya kijamii
pamoja na mabadiliko na maendeleo yake. Isitoshe, mtunzi ni mwanajamii anayetumia
lugha ya jamii kutunga kazi yake ili kuwafifikia wanajamii husika. Ukweli huu
wanaogusia waandishi hawa utategemea mtizamo, matarajio, na tajiriba za anayehusika
kwani hali mbali mbali katika jamii hutoa maana mbali mbali kwa watu mbali mbali hata
kama ni wa jamii moja. Hivyo basi ukweli hubainika tu kimuktadha.
Wale wanaosisitiza kigezo cha fasihi na jamii katika kuieleza fasihi, wametoa
kauli kwamba pana aina mbali mbali za fasihi ambazo zinachukuana na jamii
22
mbalimbali. Dhana kama vile fasihi ya kirusi, fasihi ya kiafrika, fasihi ya kiingereza n.k.
ni baadhi ya mifano ya kazi za fasihi zinazohusishwa na jamii fulani. Fasihi kama hizi
hulenga jamii fulani pana zenye kaida na maadili yanayopatana katika muundo wa
kijumla kwani katika jamii hizo huwa kuna vijamii vidogo vidogo. Kwa mfano katika
fasihi ya Kiafrika pana fasihi ya jamii ya nchi mbali mbali ambazo zimeibuka kihistoria
kwa jinsi maalum ambao ni tofauti na ya nchi nyengineo. Na katika nchi hizo pana
vijamii vingine vidogo vidogo vinavyobainishwa na lugha, mazingira, na itikadi. Hivyo
kutaja kwamba pana fasihi ya kirusi ni kutoa kauli ya kijumla tu. Vile vile pana fasihi
zinazochukuana na mifumo mbali mbali ya maendeleo ya kijamii kama vile fasihi ya
kibwanyenye, fasihi ya kisosholisti, fasihi ya kikapitolisti n.k.
Ama kwa hakika mojawapo ya majukumu ya fasihi ni kule kuihifadhi historia ya
jamii husika. Yaani kwa kuitizama kazi ya fasihi twaweza kupata picha maalum ya
historia ya jamii husika. Kwa mfano katika fasihi ya kiswahili twaweza kupata vipindi
maalum vya kihistoria. Dunia Mti Mkavu (Said A. Mohamed) ni mfano wa kazi
inayoonyesha historia ya unyonyaji na unyanyasaji wa mufumo wa ukoloni, Mashetani
(Ebrahim Hussein) ni mfano wa Kipindi cha Ukoloni-Mamboleo, na utenzi wa Al-
Inkishafi (Sayyid Nassir) ni kielelezo cha historia ya Mji wa Pate. Hivyo basi twaona
kwamba kauli kuwa


Use: 0.1091